Monday 14 January 2013

WASANII mmegeuza misiba kuwa miradi, sehemu ya maonyesho





Juma Kilowoko ‘Sajuki’.
Ipo mifano iliyo wazi. Huko nyuma tulikemea, tukadhani wameelewa lakini hivi karibuni matukio hayo yamejitokeza tena kwenye misiba ya wasanii mbalimbali iliyojitokeza mfululizo.

Baadhi ya wasanii wameonesha tabia ambayo haifai wala haipaswi kuigwa na mtu yeyote katika jamii.

Kwa kuwa kuna vyombo vya habari kwa ajili ya kuelimisha, kuburudisha na kukosoa, leo nawaambia wahusika ukweli kuwa tabia mnazozionesha wakati wa misiba hazifai na mnatakiwa kubadilika haraka iwezekavyo. Natumia lugha laini lakini kama hamtaelewa, nitafunguka vibaya.
Kila msiba unapojitokeza unaomhusu msanii mwenzenu mmekuwa na utaratibu wa kuunda kamati mbalimbali zikiwemo za mazishi, fedha, chakula na nyinginezo.


Steven Kanumba.
Sipingi kuundwa kwa kamati pindi matatizo yanapojitokeza ila ninachotaka ni kwamba mnatakiwa kubadilika kiukweli. 

Kuna baadhi yenu mnatumia nafasi hiyo vibaya hasa wale wanaoteuliwa kwenye kamati ya fedha.

Mmekuwa mkizifanya fedha za rambirambi kuwa za matumizi binafsi! Inashangaza kuona mtu anakula fedha za rambirambi. Ni aibu iliyoje? Ukweli ni kwamba huwa mnachakachua rambirambi, aidha kwa kupiga panga au kuanza kuwapigia watu simu mkiomba fedha kwa kigezo kwamba mnamsitiri mwenzenu aliyefikwa na tatizo.
Mnakumbuka kilichotokea alipofariki Steven Kanumba? Kamati ilituhumiwa sana, nikadhani wataogopa, kumbe ndiyo walikuwa wakichukua ujuzi.
Baadhi yenu mlikula fedha zilizokuwa zinakusanywa kwa ajili ya rambirambi na mwisho mkaja kuzozana wenyewe kwa wenyewe na kurushiana mpira, jambo ambalo lilikuwa ni aibu kubwa.
Ishu hiyo ilikuja kujirudia kwenye msiba wa John Maganga. Waigizaji watatu wakatajwa kuwa vinara wa kuchakachua fedha za rambirambi na haohao waliendelea kufanya hivyo hata kwenye msiba wa Sajuki kwani walijichagua tena na kuunda kamati ya fedha.


John Maganga.
Ni kitu cha kushangaza sana msanii mzima kutuma ujumbe kuwa kamati zikiundwa unaomba uwekwe kwenye kamati ya fedha. 

Ukweli ni kwamba mnajifedhehesha wenyewe, yaani mnafanya msiba kuwa mradi, hamna hata huruma na wale wafiwa.

Kwa upande mwingine jamii inawalaumu kwa tabia zenu za kujionesha kwenye misiba. Wanawake ndiyo huwa mnatia aibu zaidi, utakuta mmevaa mavazi ya hovyo yanayoonesha maumbile yenu hadharani kisha mnaanza kujipitishapitisha, usoni mkiwa mmepaka ‘mekapu’ kama vile mnaenda kwenye harusi.
Kinachoshangaza zaidi ni kuwa kumbe pamoja na ustaa mlionao bado ushamba unawasumbua, hilo lilijidhihirisha pale Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akiwapa mkono wa pole wafiwa kwenye msiba wa Sajuki, mlijipanga kwa ajili ya kumsalimia.
Mwanzoni mlikuwa kwenye mpangilio mzuri lakini ilifika mahali mkawa mnapigania kila mtu akitaka amshike mkono rais, wengine mkamng’ang’ania sijui mlitaka kubaki na mkono wake! Mpo msibani lakini mnamweleza mambo tofauti kabisa! Kwa nini msiombe nafasi siku moja mkaonana naye Ikulu? Badilikeni mnatia aibu.
Sajuki ameondoka ameacha mjane na mtoto, wanahitaji kuishi yaani kula, kulala na kuvaa hivyo wanastahili msaada mkubwa na faraja kutoka kwenu, fikisheni rambirambi zake. Acheni hizo, badilikeni for the love of game!
Kwa hisani ya GLP

0 maoni: