Saturday 19 January 2013

Utendee haki moyo wako kwa kumpenda mtu sahihi!

Naamini mtakuwa wazima wa afya njema tangu tulipoachana hapa wiki iliyopita. Ni imani yangu kuwa somo lililopita lilikuwa zuri lililokufundisha mbinu mpya za kupalilia penzi lako. Kama ndivyo ndiyo furaha yangu, maana shabaha hasa ya safu hii ni kuhakikisha walio katika uhusiano wanapata mbinu mpya za kuendelea kuwa bora kwa wenzi wao.  Ukiwa mwanachama wa kudumu wa ukurasa huu, kila tatizo litakuwa na dawa yake na mwisho wa siku kwako, mapenzi itakuwa ni shangwe siku zote za maisha yako ya kiuhusiano na hata ndoa hapo baadaye.
Leo nimekuja na mada nyingine, kama kawaida ni mada nzuri itakayokupa ufahamu mpya juu ya maamuzi yako yahusuyo mapenzi. 

Hivi ni kweli kwamba unautendea haki moyo wako? Mpenzi uliyenaye unampenda au unajilazimisha tu kuwa naye? 

Somo la leo litakupa mwanga wa kujua haki ya moyo na tamaa za mwili wako ni kipi sahihi kutendewa haki. Elewa kuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi. 

Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Mapenzi ya dhati, ambayo hayachagui fedha wala dhiki, ambayo hayatofautishi sherehe na huzuni, maradhi na faraja!

Mapenzi ya dhati, hayo ndiyo ninayoyachambua hapa katika mada yetu ya leo. Moyo wako ukubali kwa dhati na kwa hali zote kama nilivyodadavua hapo juu.

Mapenzi hayo, hukamilika baada ya wawili hao kuwa na hisia sawa za mapenzi.Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, wewe ni mtumwa wa mapenzi! Kama ndivyo, kwanini uwe mtumwa?

Unadhani hakuna mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa? Inawezekana, huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi!

Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia sana maisha yako na huyo mwandani wako! Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe!

Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda? Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwanini ujilazimishe? Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake zaidi!

Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta kuwa hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye! Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria! Mapenzi hayafikiriwi ndugu zangu!

Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako hutetemeka juu yake na hutamani uambiwe kitu fulani na huyo aliyeuteka moyo wako ghafla. 

Hii ina maana kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana, na lazima utamkaribisha! 

Huo ndiyo ukweli, moyo wako unapaswa kuwa na muamuzi wa mwisho na siyo kuingia kwenye uhusiano ukiwa huna mapenzi kwa nia ya kujifunza kupenda.

Kuna darasa la kujifunza kupenda jamani? Halijawahi kutokea kabisa, sasa hebu angalia hilo darasa la kujifunza kupenda kwanza.

Baadhi ya wasichana, akitongozwa na mwanaume ambaye anaona wazi kuwa hampendi, lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kumkubali kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume huyo. 
Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo.

“Fedha anazo, magari anayo, hata kama simpendi nitajitahidi kumpenda taratibu,” Jenny wa Magomeni anasema.
Haya ni mawazo potofu. Baada ya wazo hili kuingia akilini, huwa hana muda wa kusubiri zaidi, anakubali na wakati mwingine huweza kuingia katika ndoa ya chap chap, unadhani ni sahihi? Jibu lake hapo ni hapana.

Siyo sahihi kwa kuwa, kuna madhara yake. Kubwa ni kutokutosheka na mpenzi wako uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati, ambalo ndio msingi wa maisha. Unajua kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote.

Madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea? 

Kama hutaleta magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa, siku hiyo lazima utafukuzwa nyumbani kwa mwanaume huyo, na kama ana hasira, anaweza kukua. Fikiria zaidi juu ya siku hiyo, upo tayari kwa aibu au fedheha hiyo?

Kimsingi usijaribu kuingia katika mkumbo huu, mkumbo wa kujifunza kupenda, ni jambo gumu ambalo huweza kuharibu maisha yako kabisa. Jambo ambalo linaweza kukusababisha ukajuta kuzaliwa.

Kuwa makini, maamuzi yahusuyo mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu sana. Unapofanya uamuzi juu ya mapenzi, unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako yajayo. 

Maisha yako wewe mwenyewe, lazima ujichagulie maisha mazuri, matamu, yenye furaha yasiyo na huzuni. Uamuzi upo mikononi mwako. Unataka maisha ya aina gani? Chagua mwenyewe.


Mdau - MziziMkavu

0 maoni: