Thursday 31 January 2013

Kama utafanya haya kwa Mume au Mpenzi wako kwa Mganga huwezi kwenda ...

NI wiki nyingine tulivu tunakutana kupitia safu hii maridhawa kabisa ambapo tunazungumzia mambo kadha wa kadha yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi. Ni kona muhimu kwako wewe na wengineo wanaoyajali maisha yao kwani hakika kila utakachokisoma hapa kitakuwa ni chenye manufaa kwako. Leo nitatoa somo kwa wanawake walio ndani ya ndoa, kwenye uchumba na hata wale walio kwenye uhusiano wa kawaida.
Mwanamke anayemjali mume/mpenzi wake ndiye anayeutumia uanamke wake kutimiza wajibu, lakini wengi hujikuta wakisalitiwa au kuachwa kabisa na waume zao kutokana na ufahamu mdogo ama dharau ya mambo madogomadogo tu.


Ni busara kutambua kuwa uhusiano wa kimapenzi hauna mambo madogo. Kila kitu kina umuhimu mkubwa kulingana na nafasi yake sambamba na utekelezaji wako. 


Niwaambie kitu kimoja kwamba, usipoteze muda wako kumuendea mumeo au mpenzi wako kwa sangoma eti kutafuta limbwata la kumfanya akupende. Unapoteza muda na pesa zako bure.

Niamini mimi kwamba, ‘ukimhendo’ kwa kiwango kitakachomridhisha, tayari utakuwa umempumbuza na hatawaza kukuacha. Unawezaje? Ni kazi ndogo sana! Muoneshe unampenda na uthibitishe hilo kwa vitendo.

Daima hilo liwe akilini mwako. Mwanamke kupitia mapenzi yake ana uwezo mkubwa mno lakini lazima awe anajua kutimiza wajibu wake kwenye uhusiano. Akipatia hapo, amemaliza kazi. 

Kiukweli kabisa, kama mpenzi wako anakuacha, basi kuna mambo unayomkosea na kuyafanya mapenzi yako yageuke kuwa si lolote kwake. Unyenyekevu kwa wanawake wa kisasa kimekuwa ni kitu adimu, kiasi ambacho kimekuwa kikihatarisha uhusiano wa watu wengi.

Tambua kwamba, wanaume wanawapenda wanawake ambao hujionesha waziwazi kuwa wenyewe ni wasaidizi wao wakuu katika masuala mbalimbali. Hawavutiwi na wale ambao hupuuza mambo kwa visingizio visivyokuwa na maana.

Timiza wajibu wako kama mwanamke. Elewa kwamba wanaume wanapowekeza penzi kwa mtu flani, wanatarajia kupata liwazo la moyo. Ukipendwa halafu ukawa chanzo cha kumfanya mtu wako awe na ‘stress’, tarajia wakati wowote kuwekwa pembeni.

Mbali na hilo, wanaume pia wanapenda kuwa na wanawake wajanja kiana. Sizungumzii ujanja ule wa kupitiliza maana huenda ukawa na madhara. Sababu ya wanaume kuwapenda wanawake wajanja ni kukwepa aibu wanazoweza kuzipata pindi watakapokuwa kwenye uhusiano na washamba. 

Huogopa kujiingiza katika mapenzi na watu wasiokuwa na uelewa mpana wa mambo ambao kutokana na ufahamu wao mdogo, hujikuta wakiwa mafundi wa kuiga mambo ya kileo tena yale yaliyo hatari.

Washamba mara nyingi huwa ni malimbukeni, hujifunza mambo yasiyokuwa na faida kwa imani kwamba naye ataonekana mtu kati ya watu kumbe anaharibu. Wanawake wa aina hii ni rahisi kuwaingiza wenzi wao katika hasara kubwa. Hawakawii kuiba, ni rahisi kuharibu vitu, wao ni wabadhirifu na wanapenda makuu!

Tumekuwa tukishuhudia wanawake malimbukeni wakiiga tabia za ulevi, wakibadilika na kuwa mafuska kupindukia huku wakiwapanga mabwana kila kona. Si wameshauriwa mwanamke mafiga matatu? Ndiyo anatekeleza kwa vitendo!

Wanaporubuniwa kuwa mwanamke ni lazima awe na buzi la kuchumia pesa ni rahisi kufuata. Matokeo yake hugeuka makahaba wanaolala nyumbani, akitongozwa hakatai ilimradi aahidiwe pesa. Huku ni kuiga vibaya.

Wanawake wajanja hawawezi kuiga vitu vya kijinga, hawadanganyiki kwa penzi la pesa, wanaelewa malipo yake ni makubwa. Wakichombezwa kuhusu mabuzi hudharau na kushika hamsini zao. Ndiyo maana wanaume wanawapenda!

Jamani hili somo ni pana sana lakini kwa leo niishie hapa. Nimezungumzia ishu ya mwanamke kujitahidi kuutumia uanamke wake kumshika mumewe lakini pia umuhimu wa kuwa mjanja kidogo ili kuepukana na vishawishi ambavyo vinaweza kukuingiza kwenye matatizo.

Mdau .

0 maoni: