KUNA mambo mengine yanafanywa na wasanii wetu yanachanganya sana akili, kiasi cha kukufanya ufikiri mara mbili kama huwa wanafanya tafakuri kabla ya kusema au wanafanya makusudi kwa malengo maalum? Wakati mwingine unadata zaidi unaposikia kauli kama hizo zimetolewa na mtoto aliyelelewa katika aina ya maisha unayoamini yana maadili na vitu kama hivyo. Estelina Sanga, maarufu kama Linah, ni binti mdogo, ambaye ndiyo kwanza anaanza kuogelea katika umaarufu wa muziki wa kizazi kipya baada ya kuibuliwa pale TanzaniaHouse of Talent (THT).
Hana kazi nyingi sana alizofanya vizuri zinazoweza kukushawishi kuwa namzungumzia staa wa levo za kina Mwasiti kwa mfano. Kuna chache alizofanya mwenyewe kama Atatamani, Janjaruka, Nia yangu na baadhi alizoshirikishwa kama ile ya Barnaba, Wrong Number na ule alioshirikiana na kijana aliyewahi
kutoka naye kimapenzi, ambaye pia ni zao lingine la THT, Amini wa Mtima wangu.
Haonekani kuwa na ‘jihad’ katika kazi, kwani katika siku za hivi karibuni, amekuwa akiripotiwa zaidi katika matukio.
Siku chache zilizopita alifika ofisini kwetu na kufanya mahojiano na kituo chetu cha televisheni, kinachorusha matangazo yake kupitia mtandao, yaani Global TV Online.
Alizungumza mambo mengi yanayohusu kazi zake za kimuziki, malengo yake, changamoto bila kusahau jinsi anavyoishi na jamii inayomzunguka.
Katika mahojiano hayo, hakuondoka bila kuwaachia ‘kitu’ baadhi ya watazamaji wa televisheni hiyo, nikiwemo mimi. Alisema anapenda kuvaa nguo fupi (vimini) na zile za mpasuo kwa sababu anapenda kuliona paja lake na kwamba analipenda!
Sijui, labda wapo walioona jambo hilo la kawaida tu, tofauti na mimi. Kwangu niliitilia mashaka kauli ile, kwa sababu ina ukakasi. Kwamba analipenda paja lake, Wazungu wanasema hiyo ni obviously, yaani lazima, kwa sababu itakuwa ni kituko cha mwaka kumkuta binadamu anayechukia kiungo chake, kiwe vyovyote kilivyo.
Lakini kama mtu analipenda paja lake, kitu ambacho ni kizuri sana, ndiyo ulianike nje lionwe na kila mtu? Halafu paja ni kiungo ambacho katika mazingira na utamaduni wetu, ni nyeti. Sasa inapotokea binti mmoja, ambaye niliwahi kusikia kwamba ni mtoto wa kasisi, anasema kwamba anahusudu kuonyesha ‘live’ kiungo chake nyeti hadharani, ni lazima utilie shaka akili yake.
Akili yangu ya kawaida inaniambia kwamba mtu mwenye kukipenda kiungo chake, hasa kile nyeti, angekihifadhi, watu wasije wakakiona na kukiharibu! Kwa mtoto wa kike kama Linah, ningeamini kama analipenda paja lake kama lisingekuwa linaonekana ovyo, angelihifadhi hata kwenye baibui!
Msichana, tena aliyezaliwa mwaka 1990, anayelipenda paja lake angelificha, ili kulinusuru na wanaume wakware, wenye uchu wa wanawake wanaojianika kama Linah.
Tafsiri nyepesi kwa maneno ya nyota huyu wa Bongo Fleva ni kwamba halipendi paja lake, analionyesha kwa watu ili waliharibu.
Kama Linah anakwenda Club akiwa paja nje na pale tunajua kuna watu wenye hela zao wanaokosa watu wa kuwasaidia matumizi, unaweza kupata hisia kitu gani kitatokea?
Ni wazi kuwa analianika ili watu walione, wavutiwe nalo na baadaye ashirikiane nao kuliharibu.
Ningemshauri kama mdogo wangu kwamba wakati mwingine ni bora kukaa kimya na kuwaacha watu wakujadili wenyewe pasipo kutoa kauli zinazoweza kuwaongoza kukujadili.
Na labda, uvaaji wa nguo fupi na mipasuo tata, haiwezi kumsaidia kupandisha mauzo au uwezo wa kazi zake. Kama msanii, anaweza kuvaa mavazi hayo katika maeneo yenye kuruhusu, ambayo mara zote huwa ni usiku, lakini kuachia paja lako mbele ya kadamnasi, kwa madai kuwa unalipenda, nadhani siyo sawa.
Kwa hisani ya GPL
0 maoni:
Post a Comment