Sunday, 16 February 2014

Dk. Mahenge: Vigogo wote waliojenga kwenye fukwe kutimuliwa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Dk. Binilith Mahenge (pichani), ametangaza vita na vigogo waliojenga kwenye fukwe za bahari jijini Dar es Salaam, kuwa wataondolewa. Aidha amewatumia salama kuwa hakuna aliye juu ya sheria na kwamba wote anawashughulikia.Mahenge alitoa kauli hiyo jana muda mfupi baada ya kuzungumza na wafanyakazi na uongozi wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).Awali Dk. Terezya Huvisa aliyekuwa Waziri wa Ofisi ya Mazingira alitangaza kuwa ameshindwa kupambana na vigogo waliojenga katika maeneo hayo na kuomba msaada kwa Makamu wa Rais.

Dk. Huvisa alitoa kauli hiyo mwaka jana alipotembelea NEMC na kuzungumza na wafanyakazi na uongozi na kusisitiza kwamba kazi ya kupambana na vigogo hao ni ngumu na angeomba apate msaada zaidi.

Dokta Mahenge aliwaambia wanahabari kuwa haamini kama kuna kigogo yeyote aliye juu ya sheria na kwamba atahakikisha taratibu na sheria zinafuatwa katika ujenzi maeneo ya fukwe za bahari.

Aliwasifu wafanyakazi wa NEMC kwa kazi wanayoifanya na kwamba juhudi zaidi zinahitajika ili kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira linapewa kipaumbele.

Aliwataka wawe wazi katika suala la utoaji wa vibali kuhusu masuala ya tathimini ya mazingira kwa wawekezaji na kwamba ndani ya miezi mitatu mwekezaji awe amepata kibali chake.

Alisema ikiwa uharibifu wa mazingira utafanyika athari zake ni kubwa na kwamba taifa haliwezi kuendelea kama wananchi wataharibu mazingira.
Kuhusu uteketezaji wa taka zenye sumu, Dk. Mahenge alisema serikali inaliangalia suala hilo na kwamba kuna haja ya kununua mtambo mmoja ambao utawekwa eneo malaum ili utumike kwa kazi hiyo.

Kwa sasa taka za sumu haijulikani zinatupwa wapi na kwamba viwanda na hospitali zinaendelea kuzizalisha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bonaventure Baya alimwambia Dk. Mahenge ambaye aliongozana na Naibu wake, Ummy Mwalimu kuwa wamedhamiria kusimamia masuala ya mazingira licha ya kuwapo vitisho.

Alikiri kuwa wanapokea vitisho katika kazi zao, lakini akasema hilo haliwezi kuwakatisha tamaa katika utendaji wao wa kazi.
kwa hisani ya  NIPASHE

0 maoni: