Sunday 16 February 2014

Awilo; muziki ulimfanya akimbie shule

Kwa wapenzi na wafuatiliaji wa muziki wa Kongo,  Awilo Longomba siyo jina geni masikioni mwao. Hii ni kutokana na mbwembwe alizonazo nyota huyu awapo katika jukwaa la sanaa ya muziki. Machachari na vituko vyake vinamfanya   Awilo kuwa miongoni mwa wasanii wenye mtindo wa kipekee barani Afrika, sababu inayochangia kuwa na mashabiki lukuki.Awilo alianza kuwa na mapenzi na muziki tangu akiwa mtoto kutokana na kuhudhuria mazoezi ya muziki aliyokuwa akifanya baba yake Vicky Longomba aliyekuwa mwimbaji mkuu wa Bendi ya ‘Tout Puissant OK Jazz’.
Taratibu muziki ukaanza kumuingia kwenye damu yake na badala ya kwenda shule, Awilo akawa akitumia muda huo kupiga ngoma katika vikundi mbalimbali vya burudani.
Kabla ya kuimba, nyota huyo aliingia kwenye  muziki akiwa mpiga ngoma (tumba),kazi ambayo aliifanya katika bendi kadhaa nchini Kongo zikiwamo, Stukas, Loketo na  Viva la Musica.
Mwaka 1992, Awilo aliamua kuachana na Kundi la Viva la Musica lililokuwa likiongonzwa na Papa Wemba na kuanzisha kundi lake laNouvelle Generation.
Hata hivyo, kundi hilo halikudumu sana kwani mwaka 1995, aliamua kuanza kazi kama msanii  binafsi na hapo ndipo nyota yake ilipoanza kung’ara.
Jina la Awilo lilitawala midomoni mwa wapenzi wa burudani.
Mwaka huo huo, Awilo alifanikiwa kutoa albamu yake ya kwanza Moto Pamba, baada ya kupata msaada kutoka kwa wakongwe wa muziki Shimita, Ballou Canta, Dindo Yogo, Dally Kimoko, Sam Mangwana, Syran Mbenza na Rigo Star.
Mafanikio hayo yalimfanya Awilo kuacha kupiga ngoma na kujikita rasmi katika utunzi wa mashairi na uimbaji kazi ambayo imeendelea kumpa umaarufu mkubwa hadi sasa.
Mwaka 1998 , alitoa albamu yake ya pili , Coupe Bibamba  ambayo ndiyo ilimtangaza nyota huyo katika Bara lote la Afrika na kufanikiwa kuvuka mipaka ya bara hilo.
Pamoja na umaarufu, Coupe Bibamba ilimfanya Awilo kupata ziara za kimataifa, ambapo alifanikiwa kufika katika nchi mbalimbali za Bara la Ulaya na Amerika.
Nyota huyo aliamua kuhamia nchini Ufaransa kwa ajili ya kuendesha shughuli zake za muzikina makazi yake hadi sasa.
Mwaka wa 2008, Awilo alitoa albamu mpya aliyoiita Super man, ambayo pamoja na mafanikio makubwa katika mauzo, ilimpatia tuzo ya Mtumbuizaji Bora wa Soukous kwa mwaka 2009.

Imeandaliwa na Elizabeth Edward kwa msaada wa mtandao

0 maoni: