Wednesday 29 January 2014

Fedha za wafadhili: Serikali yaumbuka

Serikali imekiri kuwa zaidi ya Sh. 444,088,301 zilizotolewa na washirika wa maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye halmashauri nchini zimefanyiwa ubadhirifu na imewajibika kuzilipa kwa wafadhili hao. Hayo yalibainishwa jana wakati wa kikao kati ya Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, kuhusu mtiririko wa fedha za maendeleo zilizopelekwa katika halmashauri Julai mwaka jana. 
Aidha, serikali imekubali kurejesha fedha hizo zilizotumika kinyume cha malengo yaliyokusudiwa baada ya washirika hao wa maendeleo kupitia mabalozi wa nchi zinazofadhili mradi wa maboresho ya serikali za mitaa, na kuamua kwamba ufanyike ukaguzi maalumu katika eneo la usimamizi wa fedha kwenye wizara hiyo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2012. Kwa mujibu wa Waziri Ghasia (pichani), kazi ya ukaguzi ilianza Februari 18, mwaka jana na kukamilika Juni mwaka huo huo na kampuni ya Uingereza ya RSM Tenon kwa kibali cha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.


Alisema matokeo ya ukaguzi huo yalibainisha uwapo wa masula kadhaa mazuri na mapungufu na udhaifu katika kusimamia kanuni na taratibu za fedha, mkanganyiko katika ulipaji wa kodi na usimamizi hafifu wa mali za mradi ambao ulisababisha matumizi mabaya ya fedha hizo.

Ghasia alisema tayari Tamisemi iliwasilisha madai hayo Wizara ya Fedha Desemba 4, 2012 ili kuona namna ya kurudisha fedha hizo na hatua za  kinidhamu zichukuliwe dhidi ya waliohusika.

“Baada ya ripoti ya CAG, tumewasimamisha mshauri wa masuala ya fedha na mhasibu mkuu ambao walihusika kwenye mradi,” alisema.

Kadhalika, kamati hiyo iliendelea kumbana Waziri Ghasia kuhusiana na ripoti yake kushindwa kuainisha maeneo yanayolalamikiwa na wananchi kwenye halmashauri zote nchini ikiwa ni pamoja na kurejeshwa kwa madeni ya wazabuni na maboresho ya utoaji wa huduma shuleni.

Baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa sana na wananchi kwenye halmashuri nchini ni pamoja na sekta ya maji, elimu, ardhi, barabara na mawasiliano.

Pia kamati hiyo ilimtaka Waziri Ghasia kuonyesha uwajibikaji wa kuwachukulia hatua watendaji wasio waaminifu kwenye halmashauri, vinginevyo wizara yake itaendelea kulaumiwa na Watanzania kutokana kasi kubwa ya wizi wa fedha za umma.

Hata hivyo, Ghasia alisema wangeweza kuwachukulia hatua za kisheria mara moja watendaji hao, lakini sheria zinazosimamia utumishi wa umma zinawabana huku wakiwataka wabunge kwenye mikutano yao kubadilisha sheria hiyo ili waweze kuwa na mamlaka kamili ya kuchukua hatua mara moja.

MKUCHIKA ACHACHAMAA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, amesema Halmashauri za Majiji, Miji na Manispaa nchini zinakabiliwa na ugonjwa wa rushwa na kusababisha wananchi wake kuendelea kuteseka.

Pia alisema halmashauri hizo zinaboronga katika kuandaa na kupitisha bajeti hewa ambazo zimejaa rushwa na kuungwa mkono na  vikao vya ushauri vya mikoa (RCC) bila ukaguzi wa kina.

Mkuchika aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wajumbe wa kikao cha 30 cha Kamati ya Ushauri ya mkoa wa Kilimanjaro na kusema kuwa baadhi ya wakurugenzi wanatumia vibaya fedha za walipa kodi huku wananchi wakilala njaa.

Alisema baadhi ya watumishi akiwamo mweka hazina wamenyamazia na wakurugenzi kushindwa kuialika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoa elimu kwa madiwani.

“Pamoja na vikao vya ushauri kupitisha bajeti za Halmashauri na Manispaa nchini, bado wakurugenzi wezi  hawataki kuwashirikisha Takukuru katika kutoa elimu kwa mabaraza ya madiwani, hili limeruhusu kuwapo kwa rushwa katika halmashauri,” alisema Mkuchika.

"Nchi hii inatafunwa na saratani rushwa, wakurugenzi wanaogopa kuwaalika Takukuru, kwani wanajua endapo watawaalika maovu yao yatafichuliwa na madiwani. 

Hakikisheni mnawashirikisha maofisa wa Takukuru katika mabaraza yenu, kila mmoja akipambana na rushwa  mafisadi hawatakuwapo,” alisema.

Alisema kuna rushwa kubwa ambayo inawalenga wakurugenzi wa halmashauri na manispaa hasa wakati wa utoaji wa zabuni.

Kwa hisani ya  NIPASHE

0 maoni: