MWANAMKE wa nchini Uingereza, Samantha Lewthwaite, anayetuhumiwa kuhusika katika shambulio la kigaidi nchini Kenya hivi karibuni, anadaiwa kujificha hapa nchini, RAI Jumapili linaripoti. Taarifa za Samantha kujificha nchini zimeripotiwa kwa mara ya kwanza jana na gazeti moja kubwa linaloheshimika nchini Uingereza la Daily Mail. Daily Mail katika taarifa yake hiyo limeandika kuwa Samantha, ambaye kwa sasa anasakwa na vyombo vya ulinzi na usalama duniani kote, huenda akawa amejificha Tanzania au Somalia, baada ya shambulizi la Westgate Mall.
Taarifa hiyo ya Daily Mail imekuja ikiwa ni siku chache tu kupita tangu gazeti moja la hapa nchini (Siyo RAI) kuchapisha habari ya uvumi wa mwanamke aliyesadikiwa kuwa ni Samantha kuonekana katika viunga vya Jiji la Dar es Salaam.
Katika habari hiyo ambayo ilithibitishwa na polisi, ni kwamba mwanamke huyo, ambaye ni mzungu aliyefananishwa na Samantha, alifika katika benki ya Exim tawi la Tower jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuomba zabuni ya kufanya usafi.
Kauli zake tata za kuomba zabuni ya kufanya usafi, kutaka kufungua akaunti katika benki hiyo bila ya kuwa na utambulisho unaoeleweka ilisababisha baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo waanze kupata mashaka, huku wakiifananisha sura yake na ile ya Samantha.
Hatua hiyo iliibua taharuki miongoni mwa wafanyakazi wa benki hiyo na hivyo kuwalizimu kutoa taarifa polisi, ambapo Jeshi hilo Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilifanikiwa kumkamata, lakini baada ya mahojiano na kumfanyia uchunguzi walibaini si Samantha kama ilivyokuwa ikidaiwa.
Alipotafutwa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso kuzungumzia juu ya taarifa hizo za Daily Mail, alijibu kwa ufupi kuwa “Siwezi ku-realize na habari ya magazeti ya nje, nataka kufuatilia habari hiyo kwenye mfumo wa nchi na nchi kama wanavyofanya Interpol”.
Wakati huo huo, gazeti la Daily Mail limeripoti kuwa Jeshi la Polisi nchini Kenya limefanikiwa kunasa nyaraka muhimu za mwanamke huyo ambazo zina maelekezo ya kuwaandaa watoto wake kuwa magaidi.
Gazeti hilo liliandika kuwa nyaraka hizo zenye kurasa zaidi ya tisa, zinaonyesha jinsi Samantha alivyokuwa na mpango wa kufanya mauaji kwa watu wasiokuwa waumini wa dini ya Kiislamu.
Kwamba mwenendo na tabia hiyo ndio aliokuwa akiwafundisha watoto wake kuwachukia watu wote ambao ni maadui wa Waislamu.
Inaelezwa kuwa katika nyaraka hizo, aliyekuwa mume wa kwanza wa Samantha, Jermaine Lindsay, alipozungumza na watoto wake wawili kwamba watafanya nini wakiwa wakubwa, walimjibu kwamba wanataka kuwa wapiganaji wa Mujahidina.
Nyaraka hizo zilikuwa zimehifadhiwa katika sehemu salama ndani ya nyumba moja nchini Kenya, inayodaiwa kuwa ndiyo makutano yake na washirika wake kwa mipango ya kufanya mashambulizi ya kigaidi kwenye baadhi ya hoteli na vituo vya kibiashara.
Ndani ya nyumba hiyo, askari wa Kenya walikuta bunduki aina ya AK-47 pamoja na picha za watoto wa Samantha.
Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa watoto hao watafuata nyayo za wazazi wao kuwa magaidi, ambapo baba yao alijitoa mhanga kwa kulipua bomu na kuua watu kadhaa nchini Uingereza.
Samantha anatuhumiwa kuhusika na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya watalii kutoka Ulaya wakati wa sherehe za Krismasi mwaka 2011 mjini Mombasa, kabla ya hili la sasa la Westgate.
Samantha pia anatajwa kuzaa watoto wengine wawili na gaidi Habib Saleh Ghani, ambaye alikuwa mwanachama wa kikundi cha Al Shabaab.
Kwa hisani ya - Mtanzania
0 maoni:
Post a Comment