Friday 23 August 2013

Dk. Nchimbi awatimua vigogo wa polisi

SERIKALI imewafukuza kazi maofisa wanne wa Jeshi la Polisi na wengine kadhaa wakivuliwa vyeo. Maofisa hao, wanadaiwa kushiriki kwa namna moja au nyingine katika matukio yaliyotokea mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro na Kigoma. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema miongoni mwa askari hao ni wale waliohusika kutumia gari la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kusafirisha bangi katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Alisema wengine ni wale waliokamatwa na fuvu la binadamu mkoani Morogoro, ambapo walimbambikizia kesi mfanyabiashara mmoja kwa lengo la kupata fedha na mauaji ya mfanyabiashara lililotokea Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Tukio la bangi
Dk. Nchimbi, alisema katika tukio hilo, Serikali imemvua madaraka Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Arusha, Mrakibu wa Polisi, Ramadhan Giro kwa kosa la kushindwa kusimamia kikamilifu askari na maofisa walio chini yake.

Alisema pia Serikali imemsimamisha kazi Inspekta Isaac Manoni na kushitakiwa kijeshi kwa kosa la kutumiwa kumtorosha mtuhumiwa ambaye ni polisi, Edward Mwakabonga aliyekuwa dereva wa gari la FFU.

Tukio la fuvu
Katika tukio hilo, Dk. Nchimbi alisema amewavua madaraka yote Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mvomero, Inspekta Jamal Ramadhan na Mkuu wa Kituo cha Polisi Dumila, Inspekta Juma Mpamba kutokana na kuonyesha udhaifu mkubwa katika utendaji kazi wa kushindwa kuwasimamia askari wake.

Alisema kabla ya tukio la askari watatu kushirikiana na raia wawili kumbambikizia fuvu la binadamu mfanyabiashara Samson Mwita, Inspekta Ramadhan alikuwa na taarifa za mpango wa tukio hilo.

Tukio la mauaji
Akizungumzia tukio la mauaji, lililotokea Desemba 25, mwaka jana, Dk. Nchimbi alisema askari wa kituo kidogo cha polisi cha Heru Ushingo kilichopo Wilaya ya Kasulu kwa pamoja walimpiga Gasper Sigwavumba na kumweka mahabusu bila msaada wowote wa matibabu, kitendo kilichomsababishia umauti.

Alisema katika tukio hilo, marehemu Sigwavumba alipasuka bandama kutokana na kipigo na kuongeza kuwa upelelezi mbovu uliofanywa chini ya usimamizi wa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kasulu, ASP Daniel Bendarugaho kesi ya mauaji iliondolewa mahakamani.

habari NA BENJAMIN MASESE, DAR ES SALAAM
chanzo - mtanzania

0 maoni: