Monday, 3 June 2013

Kifo cha Magwea chamchanganya TID

JUMANNE wiki iliyopita haikuwa poa hata kidogo kwa Watanzania wengi wapenda burudani. Alifariki dunia Albert Kenneth Mangwea ‘Ngwea’, rapa wa Kibongo. Mbaya zaidi ishu hiyo ilitokea huko Johannesburg, Afrika Kusini au Sauzi. Ngwea na mwenzake, Mgaza Pembe ‘M 2 The P’ walipata masaibu, wakakimbizwa hospitalini lakini staa huyo wa wimbo wa Mikasi alikuwa ameshafariki dunia. Mwenzake anaendelea vizuri na matibabu nchini humo.

Hiyo ndiyo iliyokuwa hali halisi. Yawezekana mashabiki wake wameumia sana lakini kama ulikuwa hujui, yupo mtu ameumia zaidi. Ni Khaleed Mohamed ‘TID Mnyama’.

TID na Ngwea wamekuwa marafiki wa muda mrefu. Wamefanya kazi nyingi za pamoja. Ilikuwa ukimwona TID klabu ni lazima Ngwea atakuwa jirani.
Acha Top Band ya TID na timu yake. Unawajua Wanyama? Ni kundi lililokuwa likiundwa na washikaji hao wawili chini ya kampuni yao ya Radar Entertainment. Ukijiita Mnyama, ujue unawachokoza TID na Ngwea. Mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ aliwahi kuingia kwenye kashkash na TID baada ya kujiita jina hilo.


Wanyama hao wawili walikuwa na projekti zao za Unyama Unyamani, Bata Batani na Tuna-kick. Zote hizi walizifanya pamoja. Wakipanda stejini kila mwisho wa wiki, kama siyo New Maisha basi ni Billz. Nyingine nje ya Bongo.

Mbali na shoo za pamoja, jamaa hao waliwahi kukiri kwamba kazi yao ni muziki na hawafanyi kazi nyingine tofauti na muziki. Kikwazo tu kilikuwa ni wadhamini wa shoo zao.
Wanyama hawakuwa na hila ndani yao. Kama ulikuwa hujui jamaa hawa ni miongoni mwa mastaa wa muziki Bongo waliofanya kolabo nyingi hata na maandagraundi.
Katika mipango yao, jamaa hao walikuwa na lengo la kukusanya vijana wanaotafuta kutoka kimuziki ili wawaendeleze ilimradi tu wawe na vipaji vya ukweli na siyo gozigozi.


Pia kama ulikuwa hujui, Ukimwacha Juma Nature, TID na Ngwea wanaongoza kwa kuzalisha misemo mingi ili tu kuweka ‘tension’ kwenye muziki wa Bongo Fleva.

Wana majina kibao ya pamoja, Wanyama, Wala Bata, Wazazi, Majembe na mengine kibao. Walipendana sana. Unataka nikupe kisa kimoja? Ngwea alizinguana na mshikaji wake pia, Rashid Makwilo ‘Chid Benz’ wakiwa klabu pale New Maisha. Chid alitaka kumpiga Ngwea kwa sababu alimwita dogo. Basi likatokea bonge la zogo huku Chid akidaiwa kumpiga Ngwea.
Katika mtiti huo, TID alikasirika sana kwa mtu wake (Ngwea) kupigwa na Chid. Unajua kilichofuata? Kufuatia hasira aliyokuwa nayo TID akitaka kumkata mtu mitama ya shingoni kama alivyosema yeye, alijikuta akipiga ngumi kioo cha gari lake hadi kukivunja. Alikuwa yupo tayari kumtetea Ngwea kwa namna yoyote.
Jamaa wanapenda bata. Wakishazitengeneza kwenye muziki huwa wanapenda kujiachia. Kwa watoto wa mjini wanaojua kujiachia, wanafahamu ni kwa jinsi gani jamaa walikuwa wanajiachia.
Baada ya kutokea kwa tatizo na Ngwea kupoteza maisha. Nilimpigia simu TID siku ya Jumanne jioni kuhusu kifo cha Ngwea. Kwanza simu yake ilikuwa bize sana. Alipopatikana alisema: “Naomba niacheni jamani, hapa nilipo nimechanganyikiwa kabisa.”
Utakubaliana na mimi kuwa kwenye zizi amebaki Mnyama mmoja, TID, asikate tamaa mashabiki wanaukubali muziki wake. Kwa heri Mnyama Ngwea! 


Kwa hisani ya GPL

0 maoni: