Monday 28 January 2013

Mzee Small anateseka jamani .......

TUACHENI utani! Mateso ya ugonjwa unaomsumbua mkongwe wa maigizo na vichekesho Bongo, Said Ngamba ‘Mzee Small’ yamepamba moto upya ambapo kwa sasa ukimuona anavyoteseka, usipomlilia, huna huruma, Ijumaa Wikienda linakujuza. Kutoka kwenye makabrasha ya gazeti hili, Mzee Small (58), alianza kuugua ugonjwa wa kupooza au kiharusi (stroke), tangu mwaka jana ambapo alitibiwa katika Hospitali ya Amana na baadaye Muhimbili ambako madaktari walimfanyia vipimo na kugundua kuwa alikuwa na tatizo kwenye ubongo na moyo.

Kwa mujibu wa mkewe, Fatuma Said, baada ya mumewe kupimwa kipimo cha CT Scan, iligundulika kuwa kuna fundo la damu ambalo limeingia kwenye ubongo na kuganda, moyo kuwa mkubwa na tatizo la presha.

Mke huyo wa ndoa wa mkongwe huyo aliendelea kufunguka kuwa baada ya vipimo, Mzee Small alipatiwa matibabu kwa muda na kuruhusiwa kurudi nyumbani huku daktari wake akieleza kuwa atakuwa akisumbuliwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu mara kwa mara hadi damu iliyopo kwenye ubongo iyeyuke.
ASHINDWA KUHUDHURIA KLINIKI
Mama huyo alisema kuwa kwa maelekezo waliyopewa na daktari, Mzee Small alitakiwa kuhudhuria kliniki kila mwezi lakini tangu siku aliporuhusiwa hadi leo (Jumamosi iliyopita) hakuweza kwenda kutokana na kukosa fedha. Aliweka wazi kuwa pia alitakiwa kufanyiwa tena uchunguzi wa kipimo hicho cha CT Scan kwa mara ya pili lakini ilishindikana.

MAOMBI
Baada ya kukosa fedha, walijitokeza akina mama watatu na kuomba kumchukua Mzee Small kumpeleka kwenye maombi ambapo mkewe huyo aliwaambia wakazungumze naye, akikubali wampeleke kwa mchungaji huko Kibaha na kufanyiwa maombi lakini hakupona.

NDUGU WAJA JUU
Kutokana na Mzee Small kuombewa  huko, ndugu walimjia juu mkewe na kumsusia mpaka leo ambapo hakuna anayemsaidia jambo lolote kuhusiana na ugonjwa wa mumewe. Baada ya sakata hilo, mtoto wa Mzee Small, Muhidin Said, aliamua kumchukua baba yake kishari kutoka Tabata, Dar na kwenda kuishi naye Gongo la Mboto hadi sasa huku matatizo ya kuanguka na kupoteza fahamu yakipamba moto.

WASANII WAMSUSA
Ilifahamika kuwa tangu Mzee Small aanze kuugua, hakuna msanii hata mmoja aliyewahi kwenda kumuona, jambo ambalo linahuzunisha kwani walikuwa wakifanya kazi pamoja lakini sasa wakati wa matatizo wamemsusa.

SAIDIA MZEE SMALL
Ijumaa Wikienda tunaanzisha kampeni ya kumsaidia Mzee Small ambapo kwa mtu yeyote aliyeguswa, anaombwa kutuma msaada wake kwa njia ya M-PESA kwa kutumia namba ya Said Ngamba (Mzee Small) 0754647265 na TIGO PESA kwa kutumia namba ya mkewe, Fatuma Said 0658111311.


Kwa hisani ya GPL

0 maoni: