AJUAYE uchungu wa mtoto ni mzazi! Ukiwatazama akina mama watatu wa wasanii wa Tanzania waliofariki dunia kwa nyakati na sababu tofauti hivi karibuni wakilia kwa uchungu, unaweza ukadhani wazazi hao ni ndugu kwa namna nyuso zao zinavyoonekana kuwa na majonzi mazito, Risasi Jumamosi linakuchambulia.
Makabrasha ya gazeti hili yanawaonesha mama wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa, mama wa marehemu Hussein Mkiety ‘Sharo Milionea’, Zaina Mkiety na mama wa marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’, Zaituni Mzena wakilia kwa uchungu.
Wazazi hao walionekana wenye majonzi kupita maelezo kwani kila mmoja alimbeba mwanaye tumboni kwa miezi tisa, akamlea, akamtunza kwa tabu hadi akakua lakini baada ya kuanza kufaidi matunda yao tu, Mungu akawachukua.
KANUMBA
Baada ya kifo cha Kanumba Aprili 7, mwaka jana kutokea ghafla nyumbani kwake Sinza ya Vatican, Dar, mama yake mzazi alionekana akilia kwa uchungu kwani ndiyo kwanza alikuwa ameanza kufaidi matunda ya mafanikio ya mwanaye aliyekuwa kinara wa filamu za Kibongo.
Inawezekana mzazi huyo alilia kwa uchungu kufuatia madai kuwa ndiye aliyehangaika kumlea Kanumba baada ya kutelekezwa na baba yake, Charles Kusekwa.
SHARO MILIONEA
Alipofariki dunia akiwa na umri wa miaka 26 kwa ajali mbaya ya gari katika Kijiji cha Songa-Kibaoni, Muheza jijini Tanga, mama yake huyo mwenye umri wa miaka 52, alilia kwa uchungu kupita maelezo kwa kuwa msanii huyo alikuwa akielekea nyumbani kumpelekea mzazi wake huyo fedha, ikiwa ni sehemu ya kuanza kufaidi mafanikio yake lakini yakatokea ya kutokea.
SAJUKI
Alfajiri ya Januari 2, mwaka huu, haikuwa njema kwa mama mzazi wa Sajuki kwani alijikuta akilia kwa uchungu baada ya mwanaye huyo kuaga dunia akiwa na umri mdogo wa miaka 27 tu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kufuatia kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.
LAZIMA ULIE
Katika simulizi za wazazi hao za namna walivyohangaika na watoto hao hadi kufikia mafanikio alafu ghafla wakazimika kama mshumaa, hata wewe lazima ulie kwani ulikuwa ni wakati wao mwafaka wa kufaidi matunda lakini ya Mungu mengi kwani ndiye anayetoa na ndiye anayetwaa, hivyo haina budi kulihimidi jina lake.
Kwa hisani ya GLP
0 maoni:
Post a Comment